Mfahamu Mtanzania Ahmad Ally, anayejulikana kwa jina la mtandaoni kama @kakamussa, ni mpiga picha maarufu na rubani wa drone kutoka Tanzania, ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na kazi yake ya kipekee katika tasnia ya filamu. Ameweka historia, kwa kuhusika katika uandaaji wa filamu maarufu duniani ya “MUFASA The Lion King,” ambayo imeweza kuleta sifa kubwa kwa nchi ya Tanzania ikionyesha vivutio vya asili na mazingira asilia ya Tanzania.
Kwa kutumia ujuzi wake wa kupiga picha na kurekodi video kwa teknolojia ya drone, Ahmad alikuwa sehemu ya timu ya uzalishaji inayofanya kazi kwa karibu na wahusika wakuu wa filamu hii. Kazi yake imeweza kuonyesha uzuri wa mandhari ya Tanzania, na hivyo kuleta mwangaza ikionyesha mandhari ya Tanzania.

Ahmad Ally alisema, “Ni heshima kubwa kwangu kuweza kuwakilisha Tanzania katika filamu hii kubwa. Nimejifunza mengi na nina furaha kuona kazi yangu ikichangia katika kuonyesha uzuri wa nchi yetu ulimwenguni.”
Mchakato wa uzalishaji wa filamu hii ulianza mwaka 2020, ambapo Ahmad na timu yake walipata fursa ya kurekodi katika maeneo ya kuvutia kama Iringa na Ziwa Natron. “Tulirekodi vitu vingi lakini kikao cha mwisho 2020 ndio tuliambiwa tumechaguliwa kufanya ‘Mufasa The Lion King’,” anasema Ahmad. “Tulipewa fomu za kusaini ili tusiweze kushea chochote mpaka filamu itakapotoka.”
Katika uzalishaji huo, Ahmad anasema waligawanywa katika makundi matatu, ambapo walikuwemo Waafrika Kusini, Wakenya, na Watanzania. “Tul Mazingira waliyoyatumia sana ni Iringa na Ngorongoro, ambapo Ziwa Natron lilikuwa sehemu muhimu ya filamu.

Kilichomfurahisha zaidi Ahmad ni wakati walipokuwa Ngorongoro kwenye camp yao ya kulala. “Kuna Wamasai walikuwa wanalinda pale, na walikuwa wakija kutuita ‘Rafiki.’ Kumbe wale wazungu walikuwa wanacapture mazingira na wakaja kutumia jina la Rafiki ambaye ndiye yule Baboon,” alisema Ahmad kwa furaha.
Ahmad anasema, “Mimi ndiyo nimeshoot zile lsamila rocks na Motion za 360 ambazo baadaye ndio wamezigeuza kuwa Animation.” Hii inaonyesha jinsi kazi yake ilivyokuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa filamu hiyo. Baada ya filamu “Mufasa The Lion King” kutoka, Ahmad alipokea barua pepe kutoka kwa timu ya uzalishaji wakimpongeza kwa mchango wake. “Waliniandikia kunipongeza kwa kazi yangu na kusema jinsi nilivyosaidia kuleta uhalisia na uzuri wa mazingira ya Tanzania katika filamu hiyo, anasema Ahmad kwa furaha.

Ahmad Mussa hakuanzia hapo, kama unakumbuka msimu wa tatu wa Maisha Plus, kilichofanyika miaka 15 iliyopita, mashabiki walishuhudia picha za kuvutia zilizopigwa kutoka angani, zikionyesha washiriki wakipita kwenye pori kuelekea kijiji cha Maisha Plus kwa ajili ya kuanza maisha mapya ya miezi miwili. Wengi walijiuliza kuhusu teknolojia iliyotumika kupata picha hizo za kipekee, huku wakidhani kuwa kamera hizo zilikuwa kwenye helikopta.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba picha hizo zilitolewa na kamera zilizokuwa kwenye drone, teknolojia ambayo wakati huo ilikuwa bado inajitengeneza katika tasnia ya utengenezaji wa filamu na vipindi vya televisheni. Mtu aliyehusika kwa karibu na matumizi ya drone hizo ni yeye ambaye kwa sasa amepata umaarufu mkubwa kutokana na ushiriki wake katika kurusha drone kwenye ‘scenes’ zilizotumika kutengeneza filamu ya MUFASA.
“MUFASA The Lion King ” ni filamu maarufu duniani iliyotoka rasmi mwaka 2024, iliyoandaliwa na Walt Disney Picture ikiwa kama muendelezo wa filamu ya “The Lion King” ya mwaka 2019.
Hivyo, uhusika wa Ahmad Ally katika uandaaji wa Filamu hiyo ni hatua muhimu kwa Tanzania kuzidi kupasua anga Kimataifa ikiwa sehemu salama na rafiki kwa uandaji wa filamu kama hizo, Pia inatoa fursa ya kutangaza Vivutio vya asili vinavyopatikana Tanzania.
Hongera sana Ahmad Ally kwa kuipeperusha bendera ya Tanzania vyema, hakika wewe ni mfano wa kuigwa.