Mlipuko wa volkano Mlima Ibu Indonesia ya kati, umesababisha hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo. Mlipuko huo umeleta lava inayotiririka kilomita mbili kutoka kwenye kituo cha mlipuko, huku moshi mzito na safu ya moto ikionekana ikitoka juu ya shimo la volkano.
Mkuu wa Shirika la Jiolojia, Muhammad Wafid, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hali hiyo inahitaji ufuatiliaji wa karibu. “Picha zilizopatikana zinaonyesha mabadiliko makubwa katika shughuli za volkano, na tunashauri wakazi wa maeneo ya karibu kuwa makini,” alisema Wafid.
Mamlaka za eneo hilo zimeanzisha hatua za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kutoa mwito kwa wakazi kujiandaa na uwezekano wa kuhamishwa. “Ni muhimu kwa jamii kujiandaa na hatua za dharura ili kuhakikisha usalama wao,” aliongeza.
Volcano kwa sasa bado iko katika kiwango cha pili cha tahadhari. Hakujawa na agizo jipya la kuhama, lakini wageni na wanakijiji wameambiwa kuondoka katika eneo la kilomita nne hadi 5.5 kutoka kilele. Shirika hilo pia liliwataka watu kuvaa mask na miwani ya kujikinga iwapo kuna mvua ya majivu ya volkeno.
Ibu ni mojawapo ya volkeno hai zinazoendelea nchini Indonesia, ambazo zililipuka zaidi ya mara 2,000 mwaka jana. Zaidi ya watu 700,000 waliishi katika kisiwa cha Halmahera kufikia 2022, kulingana na takwimu rasmi. Indonesia, taifa kubwa lenye visiwa, hukumbwa na matetemeko ya mara kwa mara na shughuli za volkeno kutokana na nafasi yake kwenye “Ring of Fire” ya Pasifiki. Mwaka jana, Mlima Ruang katika jimbo la Sulawesi Kaskazini ulilipuka, na kuwalazimu maelfu ya wakaazi wa visiwa vya karibu kuhama.


