Utafiti mpya uliochapishwa kwenye jarida maarufu la “Science Advance”umebaini kuwa kuishi katika maeneo yenye joto kunaweza kuharakisha mchakato wa kuzeeka zaidi kuliko kuishi katika maeneo baridi.
Watafiti waligundua kuwa watu wazima wazee wanaoishi katika majimbo ya joto ya Marekani, kama Arizona, wana umri wa kibaolojia mkubwa zaidi ikilinganishwa na wenzao wanaoishi katika majimbo baridi kama Washington.
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha mabadiliko ya epigenetic katika saa za kibaolojia zinazopima kuzeeka kwa seli, ambapo mchakato huu unaonekana kuendelea kwa haraka zaidi katika mazingira yenye joto la juu. Watafiti walichunguza mambo mbalimbali ya mtindo wa maisha, kama uvutaji sigara na unywaji pombe, ili kutenga athari za joto kwenye kuzeeka.
Hata hivyo, wanasayansi wanatahadharisha kuwa utafiti zaidi unahitajika ili kutoa hitimisho kuhusu hili, kwani data iliyotumika ililenga tu watu wazima na huenda isitumike kwa makundi mengine ya watu. Utafiti huu unatoa mwanga mpya kuhusu jinsi mazingira yanavyoweza kuathiri afya na kuzeeka, na unatoa wito kwa watafiti kuendelea kuchunguza uhusiano huu muhimu.


